Monday, September 22, 2008

mwanamke wa Kiislamu ana nafasi sawa na mwanaume

na Nasra Abdallah
(Tanzania Daima,22-09-2008)

IMEELEZWA wanawake wa Kiislamu wana nafasi sawasawa na wanaume katika kutoa maoni na ushauri katika jamii.
Hayo yalibainishwa mwishoni mwa wiki na Sheikh Suleman Kivemile alipokuwa akitoa mada ya nafasi ya mwanamke kwenye kangangamono lililoandaliwa na Ofisi ya World Islamic Call Society kwa kushirikana na Baraza Kuu la Wanawake wa Kiislam Tanzania.
Alisema kuna dhana iliyojengeka katika jamii hasa ya kiislam kuwa mwanamke amekuja kumtumika mwanaume, jambo ambalo alisema halina maana yoyote.
Aidha, alisema nadharia zote zinazoonekana kumkandamiza mwanaume ni dhuluma na kuongeza kwamba ikumbukwe kuwa wanawake ndio walioijaza dunia.
“Baraza la Wanawake wa Kiislam lina wajibu wa kuhakikisha linatoa elimu kwa umma wa Kiislamu kuhusu nafasi aliyonayo mwanamke katika jamiii, kwani bila hivyo wanawake watakuwa wakiendelea kunyanyasika na kudharaulika kutokana na dhana mbaya zilizojengeka kwa jamii,” alisema Sheikh huyo.
Akizungumzia kuhusu mwanamke kubadili jina la pili pindi anapoolewa na kutumia la mumewe, alisema huo ni udhalilishaji mkubwa.
Kuhusu utamaduni wa mwanamke wakiislam kukaa eda pindi anapofiwa na mumewe na kuvalishwa nguo moja katika kipindi chote hicho, alisema dini ya Kiislamu hailikubali hilo hata kidogo.
“Hii kwa kweli katika dini haipo na ni kumnyima haki yake mwanamke kwenda kujitafutia riziki na kufanya shughuli ndogondogo za nyumbani ukizingatia kwamba baada ya mumewwe kufariki ndiye anayekuwa mzalishaji hapo nyumbani, sasa kwa kumfungia ndani atawezaje kuwatafutia watoto wake mahitaji?” alihoji.
Kwa upande wake, Naibu Katibu wa Baraza la Wanawake, Mayasa Sadallah, alisema lengo la kongamano hilo ni kuwaelimisha wanawake nafasi zao katika jamii.
Mada mbalimbali zilijadiliwa katika kongamano hilo zikiwemo mama na malezi ya jamii, ukimwi na hatari zake katika jamii, Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ibada na tabia, dhima ya mwanamke katika uzalishaji wa uchumi wa familia.