Friday, July 18, 2008

WANAWAKE NA VITI MAALUMU BUNGENI

Leo hii nimeona niimuvuzishe makala hii ambayo niliitoa katika gazeti la majira wakati wa kipindi cha kuelekea uchaguzi wa mwaka 2005,nimefanya hivi makusudi nikiamini kuwa maada hii bado ni muhimu na kuwa itaendelea kuwa muhimu katika siku zijazo hadi hapo jamii yetu itakapoepukana na mfumo dume.

KWELI VITI MAALUMU VINAWASAIDIA WANAWAKE?

Dhana ya kuwepo kwa viti maalumu kwa ajili ya wanamake bungeni imekuwa ikipokewa kwa mitizamo tofauti katika jamii.Wapo wenye mtizamo hasi dhidi ya viti hivyo ambapo wao huona kwamba kuwepo kwa viti maalumu vya wanawake bungeni ni kwenda kinyume na kaulimbiu ya haki sawa na kwamba ni kinyume na demoracia.Pia hudai kwamba viti maalumu vinamanisha kwamba mtu anachaguliwa kwa sababu tu ya jinsia yake na kwamba hali hii inaweza kuleta migogoro na hali ya wasi wasi katika jamii.

Kwa upande mwingine wale watetezi wa viti maalumu vya wanawake bungeni hudai kwamba viti malumu haviwabagui wanaume, bali vinafidia pengo la kihistoria lililopelekea mwanamke kutoshirikishwa katika maamuzi muhimu kwa muda mrefu sana.Pili ni kwamba wanawake nao wana haki ya kuwakilishwa na kuwakilisha.Tatu ni kwamba mchango wa wanawake unahitajika ili kuleta uwiano wa kisiasa.Na mwisho ni kwamba kunapokuwepo na ubaguzi wa kijinsia tunapoteza vipaji vingi muhimu katika jamii.

Sababu zote zinazotolewa na pande zote mbili ni za msingi,hivyo si busara kuzipuuza.Hata hivyo katika jamii ambazo mfumo dume umeshika hatamu kuanzishwa kwa mpango huu ni muhimu ikizingatiwa kwamba si wanaume pekee bali hata wanawake wenyewe huona kwamba kwa mwanamke kushika nafasi ya uongozi si sahihi.Ladba tujikumbushe kitu kimoja kuhusu uchaguzi wa kidemocrasia,uchaguzi wa kidemocrasia unamaanisha kwamba wale waliochaguliwa wanakuwa ni taswira ya jamii husika,yaani kwamba kama washiriki katika uchaguzi walikuwa wanaume,wanawake ,vilema na kadhalika basi miongoni mwa waliochaguliwa tunategemea kutakuwa na uwiano sawa kati ya waliochaguliwa na makundi yaliyoshiriki katika kuchagua.Inapotokea kwamba wanochaguliwa ni jinsia moja tu,yaani wanaume, basi swala hili sio la kulipuuza na hapo ndio mpango wa viti maalumu kwa wanawke unapokuwa na umuhimu wake.

Viti maalumu vinalenga kuwawezesha wanawake kushika hatamu za uongozi hivyo kuuwa kasumba ya kwamba mwanamke hawezi kuongoza.Hata hivyo ni muhimu kuzingatia kwamba mpango wa viti maalumu popote pale duniani sio ajenda ya kudumu,bali unalenga kuifanya jamii itambue kwamba wanawake wanaweza kuongoza kama walivyo wanaume ili hatimaye jamii ikishaelimika na kuwakubali wanawake kwamba wanaweza basi waachwe wenyewe wasimame kwa miguu yao wenyewe kwenye vinyang’anyiro vya uchaguzi kwenye majimbo.

Wabunge wengi wanawake wamekuwa wakiingia bungeni kutokana na kuwepo kwa mpango huu.Takwimu zinaonyesha kwamba tangu mpango huu uanzishwe mwaka 1985 hadi mwaka 2000,asilimia tisini na tano ya wabunge wanawake Tanzania wameingia bungeni kwa mpango wa viti maalumu.Mpango wa viti maalumu vya wanawake haupo Tanzania tu bali umeenea katika nchi nyingi duniani kama vile,Norway,Denmark.Sweden,Afrika Kusini,Uganda na kadhalika.Jumuiya ya SADC nayo haiko nyuma katika suala hili kwani ina azimio linalosema kwamba asilimia thelathini ya wabunge wake lazima wawe wanawake.

Baada ya kuelezea umuhimu wa kuwepo kwa viti maalumu vya wanawake katika mabunge hususani bunge letu,ni wakati sasa wa kujiuliza je katika Tanzania viti maalumu vya wanawake vinawasaidiaje wanawake wa kitanzania na watanzania wote kwa ujumla?Swali hili ni la msingi ikizingatiwa kwamba kukubalika kwa wanawake kama viongozi ndani ya jamii iliyotopea kwenye mfumo dume kunategemea ni kwa kiasi gani wale wanawake walio madarakani wameweza kuonyesha cheche zao.Je wameweza kujionyeha kivitendo kwamba wanaweza kuongoza na kujali maslahi ya jamii nzima?Je wameyashughulikiaje matatizo yanayowakabili wanawake wenzao? au je ni kwa kiasi gani wameweza kuwawakilisha wanawake wenzao?Uzoefu unaonyesha kwamba wanawake ndio wapigaji kura wakubwa.Hivyo basi ni dhahiri kwamba iwapo wanawake waliongia bungeni kwa mpango wa viti maalumu wataweza kuwawakilisha vyema wanawake wenzao basi watakuwa wamejiweka katika nafasi nzuri ya kusimama wenyewe kwenye chaguzi na kushinda kwa kishindo.Lakini kama watabakia kuwa wapitishaji hoja tu bungeni na kuwasahau wanawake wenzao itakuwa vigumu kwao kukubalika na kuaminiwa na jamii ya wapiga kura,hasa wanawake hivyo watabaki wakiomba mpango wa viti maalumu uwe ni wa kudumu kwani kamwe katika hali hiyo hawawezi kusimama peke yao kwenye chaguzi.Hali hii itawapa ushindi wa bure wale wenye mtizamo hasi dhidi ya viti maalumu vya wanawake.

Tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu mwakani kuna haja ya kuyafanyia kazi mambo mawili ambayo mwandishi wa Uganda Silvia Tamale ameyazungumzia katika kitabu chake “When Hen Begin to Crow:Gender an Parliamentary Politic in Uganda.Mwandishi huyu anaelezea mambo ambayo wanawake wanaoingia bungeni kwa njia ya viti maalumu wanapaswa kuyazingatia na kuyatilia maanani watakapokuwa bungeni.Silvia ametumia maneno mawili kuainisha aina ,mbili za wabunge wa viti maalumu ambazo jamii hasa ya wanawake inapaswa kuzitambua kabla haijapendekeza majina ya kuwania hivyo viti maalumu.Ametumia maneno “standing for”kusimama kwa niaba ya na “acting for”kufnya kazi kwa niaba ya.

Mwandishi huyu ametumia maneno standing for kumaanisha wabunge wa viti maalumu vya wanawake ambao wamo bungeni kwa sababu tu hiyo nafasi inatakiwa ikaliwe na mwanamke na wala si kwamba wanaguswa na matatizo ya wanawake wenzao.Wabunge hawa wanaoimama kwa niaba ya wanawake ni hatari sana kwani wamo bungeni kwa maslahi yao binafsi na si kuwatetea na kuwawakilisha wanawake wenzao.Kipimo cha wabunge wa ina hii wala hakihitaji elimu kubwa bali ni kujiuliza swali moja tu,je ni mara ngapi mbunge Fulani amewasemea wanawake wenzake bungeni?Kama jibu litakuwa ni hapana basi huyo hakufai,hupo tu pole kama sanamu na si muwakilishi wa wanawake, hivyo sio wa kumpendekeza kwenye uchaguzi ujao kwani wabunge wa aina hii ndio huishia tu kupiga vigelegele na kugonga meza kwa nguvu kuunga hoja za wenzao.Hata kama mfumo dume utakuwa umeota mizizi hadi bungeni bado hio sio sababu tosha ya kumzuia mbunge wa viti maalumu asiwasemee wanawake wenzake hata siku moja awapo bungeni ikizingatiwa kuwa hiyo ndio kazi aliyoendea huko.

Ni mara nyingi mambo ya kuwadhalilisha wanawake yamekuwa yakitokea na bado wabunge wanawake wakayafumbia macho.Kama wangekuwa wanayawakilisha matatizo ya wanayowakabili wanawake bungeni mara kwa mara ni dhahiri kwamba sera zinazolenga kuyatatua zingekuwa zinapitishwa na bunge na hivyo kumfanya mwanamke awe na nafasi sawa ya kuifurahia nchi yetu nzuri sawa na mwanaume.Hata hivyo simaanishi kwamba si kazi ya wabunge wanaume kuwasemea wanawake la hasha!kila mbunge ana wajibu wa kuwawakilisha wananchi wake wote waliompigia kura,lakini jukumu la kuwawakiliha wanawake bungeni linawagusa zaidi wabunge wanawake kwa sababu wao ndio wanaoelewa kwa undani matatizo yanayowakabili wanawake wenzao.Hivyo basi ni muhimu kwa wabunge hawa wanawake wakajua kuwa kazi inayowakabili bungeni ni kuanzisha hoja zitakazopelekea kutatuliwa kwa matatizo ya wanawake bungeni na si kwenda kuonyesha mitindo ya nguo zao na vito walivyosheheni miilini mwao na kudakia hoja za wenzao tu.

Mambo mengine ya kuwadhalilisha wanawake yamekuwa yakitendeka ndani ya bunge na wabunge wanawake wakakaa tu kimya hadi TAWLA,TAMWA na TGNP wapige kelele.Mifano michache ni pale spika wa bunge alipoteleza katika maongezi yake fulani na kudai watu fulani wasiwe na wivu wa kike na pale Waziri wa Elimu alipopinga swala la kuwaruhuu wasichana waliopata mimba wakiwa shule waendelee na shule akidai kufanya hivyo ni kuhamasisha umalaya,matamko ya kupinga kauli hizi hayakutoka ndani ya bunge bali nje ya bunge.Lazima wabunge watambue kwamba tmko likitolewa ndani ya bunge linakuwa na uzito wa kipakeeHii ni changamoto tosha kwa wabunge wanawake hasusani viti maalumu katika uchaguzi ujao.

Wabunge wa viti maalumu vya wanawake wa aina ya pili(acting for)ni wale ambao kabla hata hawajaingia bungeni wanakuwa tayari wana lundo la kero ambapo wakiishaingia bungeni kazi yao ni moja tu,kuzitafutia utatuzi kwa kuzianzishia hoja ambazo zitapelekea utatuzi wazo.Kwa maana nyingine ni kwamba wabunge wa aina hii hawasimami tu kwa ajili ya kuleta uwiano mzuri kati ya wabunge wanawake na wanaume bungeni kama wale wale wa kundi la kwanza(standing for)bali wapo bungeni kuwawakilisha na kuwasemea wanawake wenzao.Hawa ni wabunge wanaokerwa kweli kweli na matatizo yanayowakabili wanawake.Wabunge wa namna hii ndio wanaotakiwa katika Tanzania yetu kwani uwakilishi wao utapelekea jamii nzima kukubali kwamba kweli wanawake nao wanaweza kuongoza hivyo kuuwa kasumba ya mfumo dume,hali hii itawafanya wanawake washiriki katika chaguzi kwa miguu yao wenyewe.Hakuna shaka kwamba umanufaa wa viti maalumu utakuwa umeonekana.Ni matumaini yangu kuwa kila mbunge husika atakuwa tayari ameishajijua yupo kwenye kundi gani.Aliye kwenye kundi la kwanza huu ni wakati mzuri wa kujirekebisha ili kujiweka katika nafasi nzuri katika chaguzi zijazo.

Thursday, July 3, 2008

WACHAPAKAZI WALIOSAHAULIKA

Naomba nianze mjadala huu kwa kuwapitisha kwenye mahojiano kati ya Bwana Macdonalds ambaye ni Mwekezaji toka Uingereza na Mzee Fungameza ambaye ni mlinzi katika kampuni ya Macdonalds. ENDELEA!!!
Macdonalds:Mkeo anafanya kazi gani bwn Fungameza?
Mzee Fungameza:Hafanyi kazi Boss!
Macdonalds:Akiamka asubuhi huwa anafanya nini?
Mzee Fungameza:Huwa anatandika kitanda,kufagia uwanja,kuwapikia watoto pamoja na mimi chai,kisha kuwasindikiza watoto shule na akirudi huenda kisimani kuchota maji.
Macdonalds:Mchana huwa anafanya nini?
Mzee Fungameza:Mchana huenda kuokota kuni za kupikia na kuhakikisha chakula kinakuwa tayari watoto wakirudi.
Macdonalds:Jioni huwa anafanya nini?
Mzee Fungameza:Jioni huwa anaenda kuchota maji ,anawaogesha watoto,ananichemshia maji ya kuoga na kupika chakula cha jioni
Macdonalds: Siku za weekend mkeo huwa anafanya nini?
Mzee Fungameza:huwa anapika kifungua kinywa,chakula cha mchana,chakula cha jioni,anafua nguo zangu,zake na za watoto,anaenda shamba na …
Macdonalds:Kwa hiyo mzee Fungameza mkeo anafanya kazi gain?
Mzee Fungameza:HAFANYI KAZI BOSS NADHANI NIMESHAKUAMBIA MAPEMA
Macdonalds: MY GOD!!!

Naam, hakuna ubishi kwamba kuna watu wengi ,wanaume kwa wanawake wenye mawazo kama ya Mzee Fungameza ambao kwao kazi ni ile shughuli inayompatia mtu malipo/vijisenti ya moja kwa moja. Kwa hiyo kwao kazi isiyoambatana na malipo ya moja kwa moja sio KAZI,ila kwa kazi zenye malipo ya moja kwa moja kama kazi aifanyayo Mzee Fungameza ndio kazi bila kujali ni kiasi gani analeta nyumbani kwisho wa mwezi.Ni kwa bahati mbaya sana kwamba jamii imezipachika jina kazi zisizokuwa na malipo ya moja kwa moja kuwa ni za WANAWAKE.kwa hiyo kazi zifanyikazo majumbani kwetu kama kufua,kufagia,kudeki,kuosha vyombo,kuogesha watoto,kutafuta kuni,kuchota maji,kupika nk huonekana kuwa ni za kike.Watoto wanazaliwa katika jamii hizi na kujikuta wakiendeleza dhana hii ambayo mi naiona potofu.Ah,mama mi nikadeki kwani mimi ni mwanamke?atasikika mototo wa kiume akisema hivyo.Haishangazi kuwa wanaume walioa wakikutwa wanafanya kazi hizo huonekana WAMEKAMATWA,WAMELISHWA LIMBWATA,WAMEKALIWA nk.Inashangaza kuwa wanawake ndio huwa wa kwanza kuwashutumu wanaume (kaka zao/wadogo zao) wanapowaona wanafanya kazi hizo ‘za kike’ badala ya kuwaunga mkono na kuwapa moyo kwa ushirikiano mzuri katika ndoa zao.Lakini cha kushangaza ni pale kazi hizi hizi ‘za kike’ zinapohusisha malipo ya moja kwa moja/vijisenti, wanaume huzikimbilia,huzipora na kuzimiliki.WHY??/KWANINI???inawezekana labda sieleweki! Nina maanisha UDOBI (iwe dobi wa mtaani au dry cleaner-huku ni kufua nguo),UPISHI MAHOTELINI-kupika ni kupika tu,UUZAJI MAJI MITAANI-huku ni kuchota maji,UUZAJI KUNI NA MKAA-huku ni kutafuta kuni,UFAGIZI MASOKONI/BARABARANI/MAOFISINI-huku nikufagia N.K.Tuko pamoja?kwa hiyo hapa swala la kazi za ‘kike” wala kazi za ‘kiume’ halipo.kilicho dhahiri ni kwamba jamii haiheshimu kazi kubwa wazifanyazo dada/mama(hasa wa vijijini) zetu kutwa nzima bila kupumzika.Ukitaka kujua kuwa wanawake huchangia kiasi kikubwa sana cha pesa katika maendeleo ya familia zetu basi ajili watu/mtu wa kufanya kazi zote anazofanya mwanamke kwa siku nyumbani halafu uone utachajiwa kiasi gani.Hapo utaona ni kiasi gani cha pesa huyu kiumbe jasiri amekiokoa.Karibuni wadau,mjadala uko wazi,mawazo yenu ni muhimu katika katika kuondoa fikra potofu iliyojikita katika jamii yetu ya kutoheshimu mchango wa wanawake(hasa mwanamke wa kiafrika) katika maisha yetu ya kile siku…welcome